Imeandikwa na Farai Shawn Matiashe
MUTARE, Zimbabwe (IDN) – Unyanyasaji kupitia mtandaoni na kunyanyaswa kimapenzi mtandaoni ni miongoni mwa matatizo yanayowakumba wanawake vijana wanaojaribu kuinuka katika nafasi za kisiasa za Zimbabwe zinazotawaliwa na mfumo wa ukiume wa wanaume.
Kitu kilianza kama mjadala katika chama cha upinzani, Citizens Coalition for Change (CCC) kikiongozwa na mwanasiasa kijana na mchangamfu Nelson Chamisa kisichokuwa na miundo kiliishia na msemaji wake CCC Fadzayi Mahere kupigana mahakamani na unyanyasaji wa mtandao kutoka kwa wafuasi wa chama tawala, Zanu PF.
Mhariri wa zamani wa gazeti linalomilikiwa na Serikali, Sunday Mail, Edmund Kudzayi alitishia kuwachilia picha zilizo uchi za Mahere na wanaume wanaodaiwa kuolewa naye.
Mawakili wa Mahere baadaye walimshtaki Kudzayi kwa kumharibia jina wakitaka fidia ya $100,000 katika Mahakama Kuu ndani ya mji mkuu wa Harare.
Kesi yake ni marudio ya wanawake wengi katika siasa za Zimbabwe ambao mara nyingi huitwa majina ya madharau na kushutumiwa kuwa na kashfa za kingono na wanaume walioolewa katika jitihada za kuwanyamazisha.
“Unyanyasaji wa mtandaoni unasalia kuwa moja ya sababu zinazowafanya wanawake kujiepusha na siasa,” asema Sitabile Dewa, mkurugenzi mtendaji katika. Women Academy for Leadership and Political Excellence, shirika linalotetea haki za wanawake katika siasa.
“Limetumika kama zana dhidi ya wanawake. Wanawake wengi walio katika nyadhifa za uongozi za kisiasa na wanaowania kushika nafasi za uongozi wamekumbwa taarifa zao za kibinafsi kuvujwa mitandaoni, miili yao ikiaibishwa na wakiwa na wenzao wa kiume ili kuwapaka matope kwa wananchi kama mikakati wa kuwafanya wapoteze kura au wajitoe kwenye siasa. ”
Dewa anasema matamshi ya chuki kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na tovuti za kublogu kwa njia ya mtandao ya Twitter, majukwaa ya kutuma ujumbe Facebook na WhatsApp pia yametumika kuwasukuma mbali wanawake ndio waachane na siasa.
Barbara Gwangwara Tanyanyiwa, msemaji wa muda wa CCC Women Champions, anasema wanawake walio vijana na wanawake wengi walioolewa wanaepuka siasa kwa sababu ya unyanyasaji wa wanawake nchini.
“Cha kushangaza wanasiasa wengi wanaume wakiwemo wale ambao ni wabunge wetu hawaamini katika usawa wa kijinsia wa 50/50 kwani wanadhani ni kuwapa wanawake nyadhifa kibwelele.”
“Kwa upande mwingine, watu sasa wanachukua siasa kama taaluma, kwa hivyo wanaume hawatawaacha wanawake kuchukua nyadhifa wanazofikiria zinapaswa kujazwa na wao.”
Linda Masarira, mtetezi wa haki za binadamu na rais wa chama cha upinzani Labour, Economists and African Democrats (LEAD), amekuwa akiitwa majina ya madharau kwa mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Nilichogundua ni kwamba WanaZimbabwe ni wa mfumo wa kiume wa hali ya juu,” anasema.
“Uongezekaji wa wahusika kama mimi katika uchumi wa kisiasa wa Zimbabwe kulifanya wanaume wengi kutosikia vizuri. Pia katika safari yangu ya kisiasa nilijifunza kwamba mwanamke mwenye maoni yake kibinafsi ni mwanamke ambaye kila mtu anataka kunyamazisha kwa sababu wanaume wenyewe wanajua mamlaka ambayo wanawake wanayo na njia pekee ya kunyamazisha sauti ya mwanamke ni kwa kusema vibaya kuhusu riziki zao wenyewe.”
Ili kukuza usawa wa kijinsia Bungeni, Katiba ya Zimbabwe iliyopitishwa mwaka 2013 ilianzisha uwakilishi sawia katika Seneti na kufikia 2020, asilimia 48 walikuwa wanawake katika jumla ya maseneta 80.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2018, wabunge wanawake waliunda asilimia 34.57 ya mabunge mawili ya Zimbabwe, Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti ambayo yana jumla ya viti 350.
“Hali ya kisiasa kuharibika zaidi kwa wanawake mnamo 2023”
Huku ikiwa imesalia mwaka mmoja kabla ya nchi hiyo kufanya uchaguzi wake ulioratibiwa kufanyika mwaka wa 2023, wanawake katika siasa wanahofia kuwa barabara itakuwa ngumu kwa wanasiasa wengi vijana wa kike.
Wanawake waliopo siasani nchini Zimbabwe pia hupata unyanyasaji wa kingono nje ya mtandao.
Mnamo Mei 2020, Cecilia Chimbiri, mbunge Joanah Mamombe na Netsai Marova, wanaharakati watatu wa Zimbabwe, walitekwa nyara, wakadaiwa kunyanyaswa kingono na kuteswa kwa sababu ya maandamano dhidi ya kushindwa kwa serikali kutoa vifaa vya kujikinga wakati wa janga la Covid-19.
Badala ya Serikali kuchunguza suala hilo na kuwakamata wahusika, watatu hao walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kughushi utekaji nyara na hadi leo wanaendelea kupigana na mashtaka haya mahakamani.
“Unyanyasaji wa kisiasa na kunyanyaswa kimapenzi umetumika dhidi ya wanawake katika siasa. Kesi nyingi za unyanyasaji wa kisiasa na unyanyasaji wa kijinsia zimerekodiwa kwa miaka mingi na hii bado ni sababu ya wanawake kuogopa siasa,” anasema Dewa.
Tanyanyiwa anasema wanawake wanahitaji mazingira yasiyo ya unyanyasaji na mnamo mwaka wa 2023 hawataweza kushiriki katika idadi yao kubwa.
“Tukielekea uchaguzi wa 2023 sioni mazingira yakiwa mazuri kwa wanawake tukiona vurugu ambazo tayari zinafanywa na Zanu PF,” anasema.
Dewa anasema wakati taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa 2023, mazingira ya kisiasa yanazidi kuwa tete huku kampeni za vyama vya siasa zikiendelea nchini kote.
“Kesi za unyanyasaji unaochochewa na siasa zinazowalenga viongozi wanawake zikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mitandao ya kijamii yanayolenga maisha yao ya kibinafsi. Viongozi wanawake na wanaharakati wa kike wanakabiliwa na dhuluma na unyanyasaji unaochochewa kisiasa. Hii inasababisha wanawake wachache kushiriki kikamilifu katika siasa kwani wanahofia maisha yao na ya familia zao,” asema.
Je, Sheria mpya ya Ulinzi wa Data itawalinda wanawake katika siasa?
Zimbabwe ilipitisha Sheria ya Ulinzi wa Data ambayo pia ina vipengele vinavyohusiana na usalama mtandaoni na uhalifu mtandaoni mwezi Desemba mwaka jana.
Baadhi ya mashirika ambayo yanatetea haki za wanawake katika siasa yanazingatia Sheria mpya ya Ulinzi wa Data ili kuwalinda na kuitumia kuwashtaki wale wanaowadhulumu kwenye mitandao ya kijamii.
Ili kukabiliana na unyanyasaji wa mtandaoni, Dewa anasema, kuna haja ya kuongeza ufahamu wa makosa ya unyanyasaji mtandaoni.
Anasema wanawake walio katika siasa wanapaswa kupitia mafunzo ya usalama mtandaoni ili waweze kuimarisha ustahimilivu wao dhidi ya unyanyasaji mtandaoni na kuwapa maarifa ya namna ya kushughulikia matukio hayo.
Dewa anasema iwapo mazingira ya kisiasa yatakuwa mazuri na yasiyo na vurugu, wanawake wengi wataweza kushiriki kwa uhuru na kushiriki kikamilifu katika siasa.
“Ni wajibu wa vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa mazingira ya kisiasa yanawafaa wanawake kushiriki katika siasa,” anasema.
Tanyanyiwa anasema viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini wanapaswa kukemea udhalilishaji mtandaoni [IDN-InDepthNews – 24 July 2022]
Picha: Wabunge wanawake ni asilimia 34.57 ya Bunge la Tisa la Zimbabwe. Sifa: ZimFact